TARI YATAKIWA KUONGEZA KASI YA UTAFITI
Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania (TARI) imeelekezwa kuongeza kasi katika kufanya tafiti zinazokidhi mahitaji ya wakulima ili kuongeza tija katika mnyororo mzima wa Sekta ya Kilimo.
Wito huo umetolewa tarehe 23 Februari 2024 na Naibu Waziri wa Kilimo, Mhe. David Silinde (Mb) alipotembelea Kituo cha Utafiti cha TARI Ilonga kilichopo Wilayani Kilosa, Mkoani Morogoro.
Mhe. Silinde amesema kuna hitaji la upatikanaji wa mbegu bora za kilimo kwa wakulima zenye kuendana na mabadiliko ya tabianchi na kuhimili magonjwa; hivyo kuwataka watafiti kuongeza jitihada za kufanya tafiti na usambazaji teknolojia za kilimo.
Mkurugenzi Mkuu wa TARI, Dkt. Thomas Bwana, amesema TARI wamejipanga kutafiti na kusambaza teknolojia za kilimo zenye kukidhi mahitaji huku wakiendelea kuwekeza katika kuandaa wataalamu wa kufanya tafiti zinazotatua changamoto mbalimbali za kilimo nchini.
Dkt. Bwana amesema TARI ina miundombinu ya kisasa ikiwemo maabara na mashamba ya kufanyia tafiti katika maeneo mbalimbali; na kuongeza kuwa jitihada zitaendelea kuboresha miundombinu hiyo ili kuendana na mabadiliko ya teknolojia.
Naye Mkurugenzi wa Kituo cha TARI Ilonga, Dkt. Emmanuel Chilagane ametumia fursa hiyo kuwahamasisha wakulima kuendelea kutumia teknolojia zinazogunduliwa na TARI zenye kuendana na mabadiliko ya tabianchi ili kuongeza kipato cha mtu mmoja na Taifa kwa ujumla.
Kwa upande wake Katibu Tawala, Wilaya ya Kilosa, Bi. Salome Mkinga ameipongeza TARI na kusema kupitia Kituo cha TARI Ilonga, Wilaya ya Kilosa imeongeza uzalishaji wenye tija katika mazao mbalimbali yanayostawi ukanda huo.