Skip to main content
Habari na Matukio

UNAWEZA KUWA NA CHAKULA KINGI LAKINI UKAWA NA NJAA- DKT TIZEBA

Utamaduni wa kula aina fulani ya chakula kwa aina moja tu ni miongoni mwa mambo yanayowafanya wananchi kukumbwa na njaa pindi kinapokosekana aina ya chakula kile walichokizoea.

Moja ya matatizo makubwa katika jamii ni pamoja na wananchi kuamini katika utamaduni wa aina moja ya chakula jambo ambalo halipaswi kutiliwa mkazo kwa namna yoyote.

Hayo yamebainishwa na Waziri wa kilimo Mhandisi Dkt Charles Tizeba Leo tarehe 11 Octoba 2018 wakati akizungumza kwenye mdahalo wa kuelekea siku ya chakula Dunia ambayo hafla ya kilele chake itafanyika Mjini Tunduma Mkoani Songwe tarehe 16 Octoba 2018.

Katika mdahalo huo ulioandaliwa na Shirika la chakula na kilimo la umoja wa mataifa umoja wa chakula Duniani (FAO), Mpango wa chakula wa umoja wa Mataifa (WFP), Benki ya Kimataifa ya Maendeleo ya kilimo (IFAD) kwa kushirikiana na Chuo Kikuu cha Kilimo cha Sokoine, Waziri Tizeba alisema kuwa katika kipindi hichi Kilimo cha kujikimu sio mjadala serikalini na nchi kwa ujumla bali serikali inaendelea na juhudi za makusudi kusisitiza kilimo cha biashara ili wananchi waondokane na umasikini  wa kipato.

"Na katika hali ya kawaida endapo utekelezaji wa mpango wa kuendeleza sekta ya kilimo awamu ya pili (ASDP II) ukitekelezwa ipasavyo nchi ya Tanzania kabla ya kufikia mwaka 2025 itafikia uchumi wa kati" Alikaririwa Dkt Tizeba na kuongeza kuwa

" Ni lazima tusisitize wakulima kushughulika na kilimo biashara ili waweze kumudu elimu bora, afya bora na kila kitu"

Alisema kuwa njaa haijalishi kile kinachozalishwa bali njaa ni umasikini unaosababishwa na kutokuwa na uwezo wa kupata chakula kwani kuna uwezekana mwananchi asizalishe chakula lakini akawa na uwezo wa kununua chakula chochote anachotaka.

Alisema kuwa serikali imeanza mkakati madhubuti wa kuimarisha masoko ya mazao mbalimbali ndani ya nchi sambamba na kuimarisha masoko ya nje ambapo katika Mpango wa kuendeleza sekta ya kilimo awamu ya pili (ASDP II) muhimili wa tatu ni kuboresha masoko.

“ Ndugu zangu sio kwamba hatuna chakula wakati mwingine chakula kipo lakini watu hawali vizuri kutokana na mila na tamaduni zetu za kiafrika ambapo kwa wakati wote wanawake ndio wapishi na wanaume kusalia kuwa wahemeaji (Kununua).

Kwa upande wake Naibu Makamu wa Mkuu wa Chuo cha Sokoine cha Kilimo (Utawala na Fedha) Prof Yonika Ngaga ametoa pongezi kwa waziri wa kilimo Mhandisi Dkt Charles Tizeba kwa kukubali kushiriki mdahalo huo ambao mjadala mkubwa ulihusu kujadili namna bora ya kutatua changamoto ya njaa nchini Tanzania na Barani Afrika kwa ujumla wake