Upatikanaji wa Vibali vya Kusafirisha Mazao Nje ya Nchi
Serikali leo imetoa ufafanuzi kuhusu upatikanaji wa vibali vya kusafirisha mazao kwenda nje ya nchi ambapo imesisitiza kuwa vibali hivyo vinapatikana bila gharama na hakuna urasimu wowote.
Akitoa ufafanuzi huo, Mwanasheria wa Wizara ya Kilimo Bwana George Mandepo alisema kuwa vibali vya kusafirisha mazao ya kilimo nje ya nchi, hutolewa bila gharama na kuongeza kuwa biashara hiyo inaweza kufanywa na mtu yeyote, kinachotakiwa ni mhusika kuzingatia sheria na taratibu zilizowekwa.
Bwana Mandepo aliongeza kuwa, uuzaji wa mazao nje ya nchi, unasimamiwa na Sheria ya Usalama wa Chakula iliyofanyiwa marekebisho mwaka 2009, inayojulikana kama Sheria ya Nafaka na Mazao Mchanganyiko (Serial and Other Produce Act, 2009) inayompa mamlaka Waziri wa Kilimo kutoa kibali cha kuuza mazao nje ya nchi kwa mtu mwenye vigezo.
Sheria hiyo pia, inampa mamlaka Wizara ya Kilimo , kukasimu madaraka ya kutoa vibali kwa Makatibu Tawala wa Mikoa wakati wa dharura kama ilivyokuwa katika msimu wa kilimo wa 2013/2014 ambapo Taifa lilikuwa na ziada ya kutosha.
Bwana Mandepo aliongeza kuwa, katika Sheria hiyo inamtaka mfanyabiashara kuainisha aina ya mazao na kiwango ambacho anataka kusafirisha, lengo ni kuhakikisha kuwa, Serikali inakuwa na takwimu kamili za mazao yanayosafirishwa nje ya nchi.
Baadhi ya masharti nafuu ambayo mfanyabiashara anatakiwa, kuyafuata ni pamoja na kuwasilisha taarifa zake binafsi kama Jina lake kamili au Jina la Kampuni, anuani ya makazi, au eneo analotoka na uthibitisho wa mazao anayotaka kusafirisha nje ya nchi.
Aidha, Bwana Mandepo aliongeza kuwa Mfanyabiashara wa mazao kwenda nje ya nchi atapaswa kuwa na Cheti cha ubora wa mazao husika anayosafirisha, kinachojulikana kama ‘phytosanitary certificate’ kwa mujibu wa Sheria inayosimamia ubora wa mazao (The Plant Protection Act 1997). Sheria hiyo inataka mazao yanayosafirishwa nje au kuingizwa nchini, yawe na ubora unaokubalika Kimataifa.
Bwana Mandepo alimalizia kwa kutoa wito kuwa nafasi ipo wazi kwa kila Mtanzania kuchangamkia fursa ya kusafirisha mazao nje ya nchi kwa kuwasilisha maombi ya kibali kwa Wizara ya Kilimo Chakula na Ushirika kwa ajili ya kupata kibali hicho na kwamba Mfanyabiashara anayewasilisha maombi yake, anapaswa kuambatanisha leseni yake ya biashara, cheti cha mlipakodi na awe na idhini ya maandishi kutoka Wilaya au Mkoa ambako mazao husika yanatoka.