Skip to main content
Habari na Matukio

Waziri Bashe ataja mikakati kuongeza uzalishaji chakula

Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe amesema ongezeko la bei ya vyakula la sasa halina uhusiano na ukame, kwa sababu kama utatokea utaathiri uzalishaji wa mwaka kesho.

Waziri Bashe amebainisha hayo wakati akizungumzia upatikanaji wa chakula nchini huku bei ya vyakula ikiendelea kupanda.

“Kwa hiyo ukame unaodhaniwa kutokea hauna uhusiano wowote na ongezeko la bei la sasa. Tunaposema bei ya chakula imeongezeka lazima tuwe na ulinganisho. Hata ukiangalia ripoti ya wiki iliyopita utaona gunia la kilo 100 limeongezeka bei kwa Sh400. Mwaka 2020 gunia la mahindi lilifika mpaka Sh120,000,” alisema Bashe.

Aliendelea kusisitiza kuwa kwa sasa hakuna uhaba wa chakula na kwamba hata bei za mazao zilizopanda hazizidi asilimia 10.

“Ni kweli kwa bei ya mahindi yapo maeneo ya shida kidogo ambapo bei imefika Sh700 kwa kilo, huko ndiko tunaipeleka NFRA kuuza kwa bei ya ruzuku. Serikali tumejiandaa, bei ikipanda tunaingilia kudhibiti. Tutahakikisha hakuna Mtanzania anayekufa njaa,” alisema.

Hata hivyo, alikiri kuwapo kwa ongezeko la bei kwa bidhaa nyingine kama mafuta ya kupikia, aliyosema inatokana na kupanda kwa bei katika masoko ya kimataifa.

Mikakati ya Serikali

Akielezea mikakati inayofanywa na Serikali, Waziri Bashe alisema ni pamoja na kuongeza fedha kwenye umwagiliaji ili angalau asilimia 50 za shughuli za kilimo ziwe kwenye umwagiliaji ifikapo mwaka 2030.

Alitaja pia mkakati wa pembejeo, akisema Serikali inakabiliana na ongezeko la bei katika soko la dunia kwa kuwekekeza kwenye viwanda vya ndani.

“Tuna mipango ya muda mrefu ya viwanda vya ndani kama kiwanda cha Intraform kinachojengwa Dodoma, ambacho kitazalisha tani 600,000 za mbolea kitakapokamilika.

“Pia tutaendeleza mfumo wa usambazaji wa mbolea, utakaohakikisha kuwa makosa ya ruzuku ya 2015/16 hayatajirudia kama Serikali itatoa ruzuku siku za usoni,” alisema.

Alisema pia Serikali ina mpango wa kuanzisha Mfuko wa Kujikimu, utakaosaidia wakati wa majanga, ili iwe rahisi kwa Serikali kuingilia na kutoa msaada.

“Kingine ni kutumia mazao yenyewe kutoa ruzuku kama tulivyotoa kwenye korosho. Zao hilo limejihudumia lenyewe, mkulima akapata pembejeo.

“Tumetoa ruzuku kwenye pamba karibu Sh50 bilioni wakulima wakapata mbegu, ni zao lenyewe linahudumia. Ni mfumo wa utoaji wa ruzuku ambao siyo mzigo kwa bajeti ya Serikali,” alisema.