Skip to main content
Habari na Matukio

WAZIRI BASHE ATOA MAELEKEZO KWA TBT NA TSHTDA

Waziri wa Kilimo, Mhe. Hussein Bashe (Mb) amewataka Bodi ya Chai Tanzania (TBT) na Wakala wa Maendeleo ya Wakulima Wadogo wa Chai Tanzania (TSHTIDA) kuboresha mikakati ya kukuza na kuimarisha sekta ya chai kuanzia uzalishaji hadi utafutaji wa masoko.

Mhe. Bashe ameyasema hayo tarehe 22 Novemba 2023, ofisini kwake jijini Dodoma baada ya kupokea Wasilisho la Andiko la Ujenzi wa Viwanda Saba vya Chai vya Wakulima Wadogo wa Zao la Chai hapa nchini lililowasilishwa na timu ya wataalam kutoka Bodi ya Chai Tanzania (TTB), Wakala wa Maendeleo ya Wakulima Wadogo wa Chai Tanzania (TSHTDA), Taasisi za Care International Tanzania na Shirika la  Kazi Yetu Limited. 

Waziri Bashe amesema ni muhimu kufikiria   namna bora zaidi ya kuendesha viwanda vya chai kwa kuhakikisha zinapatikana aina  bora na sahihi za umwagiliaji, uzalishaji wa mbegu na kuanza kufikiria kuboresha mashamba yaliopo kabla ya kuongeza mashamba mapya ya chai.

Waziri Bashe amewaagiza wataalam hao kuwasaidia wakulima kuongeza uzalishaji wa chai kutoka kilo 1,000 kwa hekta zinazozalishwa hivi sasa hadi kufikia kilo 2,000 kwa hekta kwa mwaka.

Kuhusu uuzaji wa chai, Waziri Bashe amewaelekeza wataalam hao kuacha kuuza kwa njia zilizopitwa na wakati, badala yake chai iuzwe kupitia mnada wa chai wa Dar es Salaam hivyo basi lazima uzalishaji wa bidhaa hiyo uendane na mahatija ya masoko. 

Kwa upande wake, Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo, Bw. Gerald Mweli ameielekeza timu hiyo ya wataalam kuhakikisha  wanafanya kazi kwa kurasimisha kila hatua kwa mujibu wa sheria na kuwa na nyaraka zote muhimu na kufuata kila hatua za kikanuni na kitaalam.

Andiko hilo liliwasilishwa na Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Kazi Yetu, Bi. Tahira Nazari, kwa niaba ya timu ya Wataalamu hao. Andiko hilo limependekeza ujenzi wa viwanda saba vya chai; ambapo vitano ni vya kusindika chai, kimoja cha Kufungasha chai kwenye makasha; na kimoja ni kiwanda cha kutengeneza vifungashio.

Naye Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Chai Tanzania, Bi. Mary Kipeja ameahidi kuwa timu hiyo itafanyia kazi maelekezo ili kukamilisha kazi ya ujenzi wa viwanda hivyo katika muda uliopangwa.