Skip to main content
Habari na Matukio

WAZIRI MKUU MAJALIWA AWAHAKIKISHIA WADAU WA SEKTA YA MAZAO YA BUSTANI KUWA SERIKALI ITAENDELEA KUJEN

WAZIRI MKUU MAJALIWA AWAHAKIKISHIA WADAU WA SEKTA YA MAZAO YA BUSTANI KUWA SERIKALI ITAENDELEA KUJENGA MAZINGIRA MAZURI YA KUFANYA BIASHARA

Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa (Mb) leo mchana Tarehe 5 Desema, 2020 amewaeleza Wadau wa mazao ya bustani (Mbogamboga, matunda, maua na viungo) kuwa Serikali itaendelea kujenga mazingira mazuri ili kuhakikisha kuwa inasonga mbele.

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amesema Serikali katika kipindi cha miaka mitano iliyopita, imepunguza na kufuta kodi na tozo 168 ambapo 114 zilihusu sekta ya kilimo na tasnia ya mazao ya bustani ikiwa miongoni mwa wanufaika wakubwa.

“Hatua hii ni muhimu katika kuhakikisha kuwa pembejeo, zana za kilimo na huduma zinapatikana kwa wingi na kwa bei ambazo wakulima na wadau wengine wanazimudu”. Amekaririwa Mhe. Waziri Mkuu Kassim Majaliwa.

Waziri Mkuu Majaliwa ameongeza kuwa suala la usafirishaji ni la msingi katika kuwezesha biashara hususan ya mazao yanayoharibika haraka kama mazao ya bustani, minofu ya samaki na nyama na kuongeza kuwa Serikali inatambua uwepo wa changamoto katika usafirishaji wa bidhaa na imejipanga kununua ndege mpya kwa ajili ya kusafirisha mazao hayo ya kilimo, mifugo na uvuvi kwenda nje ya nchi.

“Serikali chini ya uongozi thabiti wa Rais wetu Mheshimiwa John Pombe Joseph Magufuli imeweka mikakati mbali mbali ya kuboresha miundombinu nchini na kwa kuanzia Serikali imeshaunda kamati maalum inayojumuisha wataalamu wa Serikali na wale wa Sekta binafsi.”

“Kamati hiyo imeanza kuainisha changamoto za usafirishaji na za kimfumo katika bandari na viwanja vyetu vya ndege ili kufanya maboresho yanayohitajika na hivyo tuweze kutumia miundombinu ya ndani katika kusafirisha bidhaa zetu”. Amehaririwa Waziri Mkuu Majaliwa.

Wazri Mkuu Majaliwa alitumia pia fura hiyo kuziagiza Taasisi zote zinazohusika na usafirishaji wa mizigo kwa njia ya anga na bahari pamoja na Kamati iliyoundwa kusimamia zoezi hili kwa ukamilifu. Hii ni pamoja na kufanyia kazi kwa haraka mapendekezo ya Wataalamu yatakayotokana na utafiti unaoendelea kuhusu kuboresha miundombinu na mifumo ya usafirishaji.

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa ameongeza kuwa Serikali itaendelea kushirikiana Sekta binafsi kuandaa mkakati wa kitaifa wa kuyafikia masoko mbalimbali.

“Natoa wito kwa Taasisi za Serikali, Wadau wa Maendeleo na Wadau wengine wote kushiriki kikamilifu kwenye utekelezaji wa mipango hiyo pindi itakapokuwa tayari kwa utekelezaji kuanzia mwaka ujao wa fedha.” Amemalizia Waziri Mkuu Kassim Majaliwa.