Skip to main content
Habari na Matukio

Waziri Ndalichako akabidhi rasmi mashamba kwa vijana 268 wa BBT

Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Mhe. Prof. Joyce Ndalichako (Mb) leo Januari 22, 2024 amekabidhi mashamba kwa vijana 268 waliopo kwenye programu ya Building a Better Tomorrow (BBT).

Mbali na kuwakabidhi mashamba hayo, pia amekabidhi zana za kilimo na kuwataka kujikita zaidi kwenye uzalishaji mali kiufanisi huku akisisitiza kuwa mradi huo ni kati ya miradi ya kipaumbele katika Serikali ya Awamu ya Sita.

“Maono ya Mhe. Rais Dkt. Samia ya kuwezesha vijana kuwa chachu ya kuongeza uzalishaji kwenye kilimo yametimia. Mhe. Rais amekuwa akihakikisha vijana wanajiinua kiuchumi kwa kukuza ajira na kuongeza tija kwenye kilimo,” amesema Mhe. Prof. Ndalichako.

Amesema kuwa kwa kuwa programu imehakikisha vijana wanapata mafunzo, wanawezeshwa kifedha ili kuzalisha chakula cha kutosha wizara yake itazidi kuunga mkono BBT ili kuhakikisha vijana wengi zaidi wanafikiwa.

Kwa upande wake, Waziri wa Kilimo Mhe. Hussen Bashe (Mb) mbali na kuwataka vijana hao kutumia vema rasilimali walizowezeshwa  kuendeleza kilimo, pia ameitaka jamii kufahamu kuwa BBT sio mradi bali ni programu yenye malengo matatu ikiwemo kutengeneza ajira, kupunguza umaskini na kuongeza tija.

Kwa upande wake Katibu Mkuu, Wizara ya Kilimo- Gerald Mweli amebainisha kuwa kabla ya kuanza kwa program ya BBT wizara ilifanya tathimini na kugundua kuwa vijana hawalimi kwa sababu hawana ardhi ya kulimia, hawana teknolojia itakayomfanya aweze kulima wa urahisi, ukosefu wa fedha unaoweza kumpatia mtaji.

“BBT ni programu yanye mambo matatu ndani yake ambayo ni kuwachukua vijana waliopo mtaani na kisha kuwafundisha kilimo na kuwapatia mashamba, pia inashirikiana na Chuo Kikuu cha Kilimo cha Sokoine, (SUA) ambapo vijana 200 wanapewa kozi fupi na kwenda kusimamia shughuli za kilimo pia wakulima ambapo hawa ni wakulima wanaolima kila siku lakini wanakabiliwa na changamoto za masoko, ukosefu wa vifaa na elimu ya kilimo"alisema