Skip to main content
Habari na Matukio

“Wizara itaendelea kushirikiana na wadau wa Pembejeo nchini” Silinde

Naibu Waziri wa Kilimo, Mhe. David Silinde (Mb), amekutana na watendaji wa Kampuni ya John Deere na Kampuni ya Tata kujadiliana ushirikiano katika upatikanaji wa pembejeo bora za kilimo, yakiwemo matrekta.

Mazungumzo hayo yamefanyika tarehe 15 Januari 2024 jijini Dodomq, ambapo Mhe. Silinde ameeleza kuwa Wizara inatambua nafasi ya pembejeo bora za kilimo katika kukuza sekta ya kilimo na kupongeza ushirikiano huo wenye kuleta tija.

Kwa upande wake, Meneja Mauzo wa Kampuni ya John Deere katika Ukanda wa Afrika Mashariki na Mashariki ya Kati, Bw. Pritpal Singh amesema kuwa kampuni hiyo inayofanya kazi nchini kupitia kampuni ya Tata ambayo ni wakala wake, imejipanga kuboresha upatikanaji wa pembejeo bora za kilimo zinazotakiwa na wakulima nchini.

Amesema kuwa kupitia kampuni ya Tata, eneo la Kibaha Mkoa wa Pwani kitajengwa kituo maalum cha kuunganisha matrekta (tractor assembling) hatua itakayosaidia upatikanaji wa matrekta kwa bei nafuu nchini.

Pia katika maeneo ya Mtanana na Chinangali yaliyopo jijini Dodoma, kutajengwa kituo cha upatikanaji wa pembejeo za kilimo kwa ajili ya kuwahudumia wakulima wa maeneo hayo, pia vitajengwa visima vya umwagiliaji.

Amesema, katika eneo la viwanja vya Nane Nane, jijini Dodoma eneo ambalo hutumiwa na Serikali katika maadhimisho ya Sherehe za Nane Nane kanda ya kati, hapo patajengwa kituo cha mfano cha huduma za pembejeo.