Skip to main content
Habari na Matukio

WIZARA YA KILIMO INAENDELEA NA UPIMAJI WA AFYA UDONGO

Wizara ya Kilimo kupitia Idara yake ya Usimamizi na Mipango ya Matumizi ya Ardhi ya Kilimo inaendelea na zoezi la upimaji wa afya ya udongo ambapo timu ya wataalamu ipo katika Wilaya ya Ikungi, mkoani Singida kupima udongo kwenye vijiji vinne kuanzia tarehe 30 Mei 2024 hadi 6 Juni 2024.

Vijiji hivyo ni pamoja na Kijiji cha Issuna A na B, Kijiji cha Ng’ongosoro na Kijiji cha Mkiwa mbapo timu hiyo ya wataalmu inashirikiana na Watendaji wa vijiji pamoja na wananchi katika upimaji wa udongo huo.

Akizungumzia kwa undani upimaji huo, Afisa Mwandamizi kutoka Idara ya Usimamizi na Mipango ya Matumizi ya Ardhi ya Kilimo, Bi. Sauda Mohamed Mjape anasema upimwaji wa afya ya udongo unasaidia kuwa na takwimu sahihi za hali ya udongo nchi nzima hatua itakayoiwezesha Wizara kuihudumia kiufanisi sekta ya kilimo.

Amefafanua zaidi kuwa, ”upimaji udongo utasaidia kujua aina ya mazao yanayofaaa kulimwa katika shamba husika ambalo udongo wake umepimwa, pia kujua aina ya virutubishi vilivyopo kwenye udongo na vipo kwa wingi gani.  Taarifa hizi ni muhimu katika kumhudumia mkulima.”  Ameongeza kuwa kupitia taarifa hiyo mkulima atajua kiasi cha mbolea kinachotakiwa kwenye shamba, kwa kuwa mashamba mengine udongo wake hauhitaji mbolea nyingi.”

Kwa upande wake, Mtendaji wa Kijiji cha Issuna, Bi. Agnes Ringo mbali na kupongeza hatua hiyo ya Wizara ya Kilimo ya kupeleka wataalamu kwenye kijiji chake kupima udongo, amesema kuwa hatua hiyo itawawezesha wakulima kulima kwa tija ambapo watakuwa wakijua aina ya mazao ya kulima kwenye shamba husika.

Ifahamike kuwa tangu kuingia madarakani Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ameleta mapinduzi katika Sekta ya kilimo kwa kuwezesha tafiti na sayansi kuzidi kutumika kama sehemu ya kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi, kuzalisha mbegu bora na kulima kilimo cha kisasa.