Skip to main content
Habari na Matukio

WIZARA YA KILIMO YAIMARISHA MATUMIZI YA MFUMO WA KIDIGITI

Wizara ya Kilimo inaendelea na mpango wa kuimarisha matumizi ya mfumo wa kidigiti wa Crop Stock Dynamics Systems (CSDS) ili kukabiliana na ukosefu wa taarifa sahihi za mazao katika maeneo ya sokoni, maghala binafsi na vituo vya ukaguzi nchini kwa ajili ya kufuatilia kiasi cha mazao ya kilimo kilichohifadhiwa nchini.

 

Zoezi hilo limefanywa na timu ya wataalamu kutoka Kitengo cha Masoko na Usalama wa Chakula katika Wizara ya Kilimo ambapo wamefanya ukaguzi maalumu (technical backstopping) ya mfumo huo katika Kata na Halmashauri za Mikoa ya Iringa na Ruvuma ili kubaini ubora, changamoto, maeneo ya kuboresha na kuzungumza na wafanyabiashara wa mazao ya kilimo.

 

Bi. Limi Thomas, Afisa Kilimo wa Halmashauri ya Manispaa ya Iringa ameeleza kuwa hadi sasa wamefanikiwa kusajili maghala 22 kati ya maghala 42; Masoko matatu (3) pamoja na Kituo cha Ununuzi wa Mazao kimoja (1) yanayopatikana kwenye Halmashauri yake na kuongeza kuwa mfumo umeendelea kurahisisha kazi ya utumaji wa taarifa ukilinganisha na ilivyokuwa awali kwa njia ya karatasi.

 

Aidha, Bw. Thadei Mbele Afisa Kilimo wa Halmashauri ya Madaba Mkoani Ruvuma amesema kumekuwa na changamoto ya mtandao katika kuendesha mfumo pia ushirikiano mdogo kutoka kwa wafanyabiashara wa mazao ya kilimo wakihofia taarifa zao kupelekwa Mamlaka ya Mapato (TRA) hali ambayo imechagiza kasi ya usajili kuwa ndogo.

Wafanyabiashara wameishukuru Serikali kwa kupatiwa elimu ya mfumo ili kuendelea kutoa taarifa sahihi zitakazosaidia kuikuza Sekta ya Kilimo kufikia malengo ya Ajenda 10/30.

Timu ya Wizara imetoa wito kwa Maafisa Kilimo wote waliopata mafunzo ya mfumo huo kuendelea kutoa elimu kwa maafisa ugani katika ngazi ya Kata ili kuendelea na zoezi la kusajili vituo vya ununuzi wa mazao, maghala za sekta ya umma, sekta binafsi na vyama vya ushirika ili kuisaidia Serikali kufuatilia kiasi cha mazao ya kilimo kilichohifadhiwa.

Mikoa mingine iliyofanyiwa ukaguzi ni Rukwa na Katavi ambapo Wizara inatarajia kufanikiwa kwa mfumo huo kutawezesha shughuli za biashara ya kilimo na kuhakikisha upatikanaji wa takwimu sahihi za chakula kwa ajili ya usalama wa chakula nchini.